WAZIRI
MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi wa vitengo na wakuu
wa taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) wapate nakala ya
hansard ya hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la
11, waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha.
“Katibu Mkuu hakikisha umepata
hansard ya hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge na
uhakikishe kila mkurugenzi ana nakala na kila mmoja wenu lazima
ahakikishe anafanyia maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameyaainisha. Ni
lazima tuelewane ni nini tunapaswa tufanye,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumanne, Novemba 24, 2015) wakati akizungumza na wakuu wa taasisi,
wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwenye
mkutano uliofanyika ofisi ndogo ya TAMISEMI, barabara ya Kivukoni,
jijini Dar es Salaam.
“Ninatamani kuona mabadiliko ya
utendaji kazi Serikalini katika kipindi kifupi. Natamani kila mmoja
asiridhike na uzembe unaofanywa huku chini. Ni nyote ni wataalamu, kwa
hiyo mnapaswa kudhirisha elimu yenu na ujuzi mlionao,” aliwasisitizia
Wakurugenzi hao.
Alisema kila mkurugenzi na mkuu wa
taasisi anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi kwenye sekta
yake kwani hilo litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya kuona
mabadiliko ya utendaji kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. “Ninyi
wakurugenzi siyo desk officers bali ni field officers. Nataka muweke
utaratibu wa kwenda vijijini mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu,
uaminifu na weledi wa kazi,” alisisitiza.
“Mambo ninayotaka mhimize
watendaji waliopo chini yenu ni pamoja na haya yafuatayo: muda wa
kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa kukaa kazini uzingatiwe, utokaji
kazini kwenda kwenye chai na chakula cha mchana udhibitiwe, na mipango
na malengo ya kazi kwa siku ni lazima yafikiwe,” alisema.
“Tunataka kujua mtumishi amefanya
nini tangu alipoingia ofisini. Suala siyo kukaa tu ofisini, kwani kuna
mtu anakaa ofisini, hajaenda hata kunywa chai lakini ukiuliza amefanya
nini hupati jibu la kueleweka. Sisi kama vongozi wao ni lazima tujue
wanafanya kazi gani wanapokuwa maofisini,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
Majaliwa ameitisha kikao ofisini kwake kesho saa 4 asubuhi akitaka
kupatiwa taarifa ni kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART)
haujaanza kazi hadi sasa. “Kesho saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi
Mkuu DART na watendaji wako mje ofisini. Nataka kupata maelezo ni kwa
nini mabasi hayajaanza kazi hadi leo, je ni lini yataanza kazi, je ni
nani anakwamisha. Na hata kama ni sheria, ni kwa nini tusiziharmonise
ili kuondoa hivyo vikwazo,?” alihoji Waziri Mkuu.
“Ninataka kupata haya maelezo kwa
sababu Watanzania na hasa wana-Dar es salaam, wamesubiri kwa muda kuona
mradi ukianza kazi ili uondoe kero ya usafiri. Wao wanajua anayehusika
ni TAMISEMI,” aliongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na watumishi na viongozi wa TAMISEMI, Katibu Mkuu wa
OWM-TAMISEMI, Bw. Jumanne Sagini alimweleza baadhi ya mafanikio na
changamoto ambazo wizara hiyo imekabiliana nazo katika utendaji wake wa
kazi.
Kuhusu ujenzi wa vyumba vya
maabara kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, Bw.
Sagini alisema vyumba hivyo vimeongezeka kutoka 247 mwaka 2005/2006 na
kufikia 6,161 mwaka 2014/2015. Pia alisema vyumba 4,228 viko kwenye
hatua za kukamilika ujenzi wake.
Kuhusu utengaji wa madirisha ya
kuhudumia makundi yenye msamaha kama wazee na watu wenye ulemavu
hospitalini na kwenye vituo vya afya, Katibu Mkuu alisema nayo
yameongezeka kutoka madirisha 5,074 mwaka 2010 na kufikia 7,903 mwaka
2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 55.
No comments:
Post a Comment