SERIKALI imewasimamisha kazi
watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao jana
iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani.
Watumishi hao ni Bw. Anangisye
Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni.
Uamuzi huo umetolewa leo
(Jumamosi, Novemba 28, 2015), na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa
ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazowakabili.
Kama ilivyo kwa
wenzao sita waliosimamishwa kazi jana (akiwemo aliyekuwa Kamishna Mkuu),
nao pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi
utakapokamilika.
“Kazi ya kuwachunguza ilianza
jana ileile na sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi
ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi,” alisema Waziri Mkuu.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu
Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa
kuwaandikia barua watumishi hao.
Jana mchana, Waziri Mkuu alifanya
ziara ya kushtukiza kwenye bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya
kukagua namna shughuli zinavyoendelea kwenye bandari hiyo hasa kwenye
maeneo ya kupokelea mizigo kutoka nje ya nchi.
Katika kikao kilichofanyi ka
bandarini hapo na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Waziri
Mkuu aliamua kuwasimamisha kazi maafisa watano na TRA kutokana na
‘upotevu’ wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Waziri Mkuu alisema upotevu huo
unasababishwa na mchezo unaofanyika baina ya wafanyabiashara na
watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru
na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
No comments:
Post a Comment