National Arts Council BASATA
PUBLIC NOTICE
BASATA LATAKA KUONDOLEWA/KUSITISHWA MARA MOJA KUCHEZWA KWA NYIMBO ZOTE ZENYE KUKENGEUKA MAADILI, SHERIA NA TARATIBU
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
linawaagiza wasanii, wamiliki na waendeshaji wa wavuti, tovuti na vyombo
vya habari hususan radio na runinga kuondoa na kuacha mara moja kurusha
au kutangaza au kucheza nyimbo zote zenye maudhui ya kashfa, matusi,
kejeli, udhalilishaji ambazo zinahatarisha kuigawa jamii ya kitanzania
katika misingi yoyote hasa katika kipindi hiki Taifa linapoendelea na
kampeni za kisiasa na kujiandaa na uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa kifungu namba 118
(a-d) cha Sheria ya Bunge namba 9 ya Mawasiliano ya Mtandao ya mwaka
2010 ni marufuku kwa njia yoyote kwa mtu au chombo chochote kutengeneza,
kuzalisha, kusambaza au kutangaza ujumbe ambao una mlengo wa matusi,
dharau, uzushi au jinai kwa lengo la kutukana, kutisha, kusumbua au
kushusha hadhi ya mtu mwingine.
Aidha, Sheria ya Bunge namba 4 ya
Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 45 (1) (a-c) kinatoa mamlaka
kwa taasisi au mtu yeyote anayebaini uvunjifu wa Sheria katika mitandao
kutoa notisi kwa yeyote yule anayesambaza au kutangaza ujumbe au
maudhui yanayovunja sheria za nchi kuacha mara moja au vinginevyo hatua
za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayekaidi.
Ni kwa msingi huu, BASATA
linawaagiza wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na wale wenye akaunti
kwenye mitandao ya kijamii kama sound cloud, U-Tube, ITunes nk. kuondoa
ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya kwanza ya taarifa hii nyimbo zote
zinazokengeuka maadili na kubeba mlengo wa matusi, kashfa, kejeli na
udhalilishaji wa watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa na
kitaifa.
Aidha, BASATA linawakumbusha tena
Wasanii wote nchini kuacha mara moja kubuni na kutengeneza kazi za Sanaa
zenye kuashiria kuigawa jamii katika misingi yoyote ya kibaguzi na
zaidi kutumia Sanaa kubomoa jamii badala ya kuijenga.
BASATA linawasisitiza wamiliki wa
vyombo vya habari hususan radio na runinga pia watangazaji na Ma DJs
kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza maudhui yoyote ya Sanaa yenye
mlengo wa kuibua chuki, matusi, kashfa na mgawanyiko wa Taifa.
BASATA kwa mamlaka yake chini ya
Sheria namba 23 ya mwaka 1984 na yale ya Sheria ya Mawasiliano ya Posta
na Mitandao ya mwaka 2010 na ile ya Makosa ya mitandao ya mwaka 2015 kwa
kushirikiana na vyombo vya dola halitasita kuchukua hatua kali za
kisheria na kinidhamu kwa wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na vyombo
vya habari ambavyo vitaendelea kutangaza na kusambaza nyimbo zenye
mwelekeo wa kuhatarisha usalama, umoja na mshikamano wa Taifa.
BASATA likiwa ni msimamizi na
mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linatambua kwamba Sanaa ikitumiwa kwa
ukengeufu inaweza kuwa chanzo kikuu cha machafuko, mivurugano na kupotea
kwa amani nchini. Hivyo umakini unahitajika miongoni mwa wasanii katika
kuzingatia weledi, maadili, uzalendo kwa taifa na kuitumia Sanaa kama
chombo cha kujenga jamii yenye kuzingatia maadili.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment