by John Bukuku on August 6, 2015
Sisi kama Chama
tumezipokea taarifa hizo na tunayaheshimu maamuzi yake. Ni haki yake ya
kikatiba na haki ya kidemokrasia kufanya maamuzi anayoyaona yana maslahi
kwake.
Bila shaka, Profesa
Ibrahim Lipumba amekifanyia kazi kubwa Chama chetu katika miaka 16
ambayo alikuwa Mwenyekiti wetu, nafasi iliyomfanya awe kiongozi wetu
mkuu. Kwa nafasi yake hiyo, pia ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa
demokrasia katika nchi yetu. Tunaithamini kazi hiyo na tutaendelea
kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa kwa Chama chetu na nchi yetu.
Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ya baadaye.
Chama Cha Wananchi
(CUF) ni taasisi na kinaendeshwa kitaasisi. Ndiyo maana maamuzi yake
yote yamekuwa yakifanywa kitaasisi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za
Chama. Kwa msingi huo, pamoja na ukweli kwamba kuondoka kwa Profesa
Lipumba katika safu ya uongozi kutaacha pengo hasa katika kipindi hichi
ambacho tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tunawahakikishia wanachama na
wapenzi wa CUF na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba Chama hichi
hakitayumba.
Katika historia yake,
CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi lakini mara zote
kimeonesha uwezo mkubwa wa kuhimili dhoruba na misukosuko hiyo na
kukabiliana na athari zake. Hatuna chembe ya wasiwasi kwamba hata
mtihani huu tutauvuka na tunaamini tutaibuka tukiwa Chama imara zaidi.
Katibu Mkuu ameagiza
kuitishwa kwa vikao vya dharura vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa siku ya Jumapili, tarehe 9 Agosti, 2015
ili kujadili hatua hiyo na kufanya maamuzi juu ya hatua muafaka
zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi hiki hadi hapo Chama
kitakapomchagua mwanachama mwengine kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti.
Katika kipindi hiki,
Chama kinawataka wanachama na wapenzi wake wote kuwa watulivu na
wavumilivu na kusubiri maelekezo ya vikao vya juu vya kitaifa vya Chama.
Mwisho kabisa,
tunawahakikishia wanachama wetu na Watanzania wote kwa ujumla kwamba CUF
itaendelea na shughuli zake kama Chama na pia kama mshirika katika
UKAWA ambayo CUF ilikuwa ni katika waasisi wake. Tunawahakikishia
wanachama wetu na Watanzania wote kwa ujumla kwamba CUF itatumia nguvu,
uwezo, juhudi na maarifa yake yote kuhakikisha kwamba inaulinda UKAWA
ambao unaonekana kuwa mwiba kwa CCM. Tunatambua kwamba kuna njama na
mbinu kubwa na nyingi zinazofanywa na watawala kutaka kuuvuruga na
kuuhujumu UKAWA wakidhani kwamba watapata manusura. Tumesema na
tunaendelea kusema CCM mwaka huu hawana manusura. Watanzania wameamua
kuwan’goa, na watan’goka Tanzania Bara na Zanzibar kupitia sanduku la
kura tarehe 25 Oktoba, 2015. Wimbi hili kubwa la mabadiliko halizuiliki
tena.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAWASILIANO NA UMMA
06 AGOSTI, 2015
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAWASILIANO NA UMMA
06 AGOSTI, 2015
No comments:
Post a Comment