Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Sunday, February 1, 2015

WAZIRI MKUU ATAKA VETA IANDAE VIJANA STADI YA MADINI


*Akabidhi vyerehani 20 kwa wahitimu wa VETA Songea

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Bodi ya Mamlaka ya Vyuo.Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini uelekeze jicho lake Nyanda za
Juu Kusini na kuandaa vijana wenye weledi na stadi ya uchimbaji madini
ili kukabili changamoto za soko.

Ametoa wito huo jana jioni (Jumamosi, Januari 31, 2015) wakati
akizungumza na walimu na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA) cha Songea mjini, mkoani Ruvuma ambako pia alikabidhi vyerehani
20 vyenye thamani ya sh. milioni 4/- kwa wanafunzi 20 waliohitimu kozi
ya ushonaji mwaka jana.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Songea mjini jana jioni akitokea Dodoma,
alifanya kazi hiyo ya kukabidhi vyerehani ikiwa ni utekelezaji wa
ahadi aliyoitoa Julai 20, 2013 wakati akizindua chuo hicho alipofanya
ziara ya kikazi kwenye mkoa huo.

“Katika kipindi kifupi, mkoa wa Ruvuma umeanza kubadilika kwa kasi ya
haraka. Kuna madini ya urani, makaa ya mawe na dhahabu. VETA inapaswa
iangalie fursa hii kwa kuandaa vijana wenye stadi za uchimbaji madini
ili wakati wawekezaji wakianza kuchimba tayari muwe na watu wa kufanya
hiyo kazi kutoka kwenye mkoa huu,” alisema Waziri Mkuu.

“Wasilianeni na Wizara ya Nishati na Madini ili mjue mahitaji yao
kwenye eneo hili ni yapi. Wakianza uchimbaji watataka watu wa kufanya
kazi hizo. Andaeni vijana... siyo mkae tu na kuja kushtukizwa au
mjikute vijana kutoka mbali wanapata hizo ajira wakati wa kwenu
wangeweza kunufaika na fursa hii,” alisema.

Aliwataka vijana wanaosoma katika chuo hicho wasome kwa bidii na
kuacha kasumba ya kuchagua kazi na kuonea aibu baadhi ya kazi.
“Someni, someni sana kwa sababu ustawi wa maisha ya Mtanzania hapo
baadaye unategemea elimu ya ufundi. Tuachane na fikra potofu za
kuchagua kazi. Kama ni mpishi fanya kazi ya upishi vizuri sababu
walaji wapo, hawaishi,” alisisitiza.

Alisema VETA inaweza kuwa suluhisho la ukosefu wa ajira hapa nchini
kwa sababu ufundi na stadi wanazopata wahitimu wa vyuo hivi vinapaswa
kuwapatia ajira. “Tanzania ina wakazi milioni 45 na wote hawa wanataka
kuvaa. Mkianzisha kikundi kidogo kuamua kushona tu sare za shule,
tayari mtakuwa mmetoa jibu kwa hitaji la sare za wanafunzi. Wamachinga
watanunua kwenu na kuuza lakini na ninyi pia mtapata fedha kuendeshea
mradi wenu,” aliwasisitizia wahitimu hao.

Mapema, akisoma risala ya chuo hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Kanda
ya Nyanda za Juu, Bw. Kabaka Ndenda alisema chuo hicho kimekwishatoa
wahitimu wa kozi fupi 2,627 katika fani mbalimbali za mafunzo ambapo
kati yao wavulana ni 2,202 na wasichana ni 425.

Aliiomba Serikali iiangalie VETA kisera zaidi kama mkombozi wa ajira
hasa wakati huu ambapo vijana wengi wanakabiliwa na ukosefu wa ajira.
Alizitaja baadhi ya kozi zinatoloewa chuoni kuwa ni mafunzo ya udereva
wa magari na pikipiki; uhazili; utengenezaji wa kompyuta; umeme wa
jua; umeme wa majumbani; ulimbwende (cosmetology) na upishi.

Alisema chuo hicho kwa sasa kina wanafunzi 298 wanaoendelea na kozi
mbalimbali na mwaka huu kinatarajia kudahili wanafunzi 306.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI MOSI, 2015.

No comments:

Post a Comment