| Jaji Mary Shangali |
| Akikagua gwaride maalumu wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini, mjini Iringa |
| Wakili wa Serikali Mfawidhi, Abel Mwandalama |
| Wakili Lwezaula Kaijage, mwakilishi wa TLS |
| Burudani za nyoka zilikuwepo |
| Baadhi ya waalikwa walioshiriki maadhimisho hayo |
| Kwaya nayo ilikuwepo |
| Mchezo wa kuchezea kofia |
WAKATI wiki ya sheria inchini ikiendelea ,jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Iringa, Mary Shangali amesema serikali ina wajibu wa kuhakikisha
wananchi wanapata huduma za kimahakama bila vikwazo vya kiufundi wala gharama
kubwa za ada au malipo ya mawakili.
Shangali aliyasema hayo kwenye sherehe ya
kuadhimisha siku ya sheria nchini iliyofanyika mahakamani hapo juzi.
Mbele ya waalikwa mbalimbali wakiwemo
viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini, alisema serikali inapokubali
kupitisha au kuwepo sheria zenye vikwazo au masharti mengi kama zilivyo baadhi
ya sheria za uchaguzi inawanyima wananchi fursa ya kupata haki zao.
Akitoa mfano alisema kutungwa kwa kifungu
cha sheria kilichomtaka mlalamikaji katika kesi ya uchaguzi kuweka mahakamani
dhamani ya Sh Milioni 5 kabla kesi haijapokelewa na kupangiwa tarehe ya
kusikilizwa kilionekana kuwafungia walalamikaji mlango wa kupata haki.
Jaji huyo alisema serikali ina wajibu wa
kuhakikisha huduma ya kimahakama inapatikana karibu na wananchi au kwa maeneo
mengine wanaifikia kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Alisema kuondolewa kwa vikwazo au
masharti mengi ya kupata haki na uwepo wa mahakama huru na imara utasaidia kulinda
demokrasia na utawala wa sheria kwa kuzingatia Katiba.
Katika utekelezaji wa kuboresha huduma ya
utoaji haki, aliishukuru serikali akisema imeendelea kuzipitia na kuziboresha
sheria na hivi karibuni imeanzisha mifumo ya huduma ya msaada wa kisheria ili kusaidia
wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria kulingana na uwezo wao wa kipato.
“Serikali imeendelea kuzipitia sheria
zinazohusu uendeshaji na mwenendo wa kesi ili kuondoa vikwazo vinavyozuia
upatikanaji wa haki na ili kuongeza idadi ya wataalamu, vyuo mbalimbali vyenye
mikondo ya sheria vimeanzishwa,” alisema.
“Aidha serikali iliazimia kuiondoa
mahakama ya Tanzania katika wingu la muda mrefu la bajeti finyu na kuanzisha
mfuko maalumu wa mahakama. Kitendo hicho kinaelekea kufanikisha mabadiliko na
maboresho yanayofanywa na mahakama ya Tanzania,” alisema.
Awali Wakili wa Serikali Mfawidhi, Abel
Mwandalama alisema ili nchi iwe na amani na utulivu ni wajibu wa serikali kama
mtendaji mkuu, kusimamia vizuri sheria na kutekeleza maagizo ya bunge na
mahakama.
“Katika kutekeleza wajibu huo serikali
haina budi kutenda haki kwa wananchi wake wote bila upendeleo wowote,” alisema.
Alisema kutokana na tafiti mbalimbali
zilizofanyika barani Afrika imebainika kuwepo kwa uvunjifu mkubwa wa haki za
binadamu kwenye mchakato mzima wa mfumo wa haki jinai ikilinganishwa na mfumo
wa haki madai.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Lwezaula Kaijage ili kuwasaidia wananchi wasiojiweza chama
hicho kimeanzisha utaratibu wa kutoa msaada wa kisheria bure.
No comments:
Post a Comment