Kwa
muda sasa kumekuwapo na tuhuma zinazohusu "wizi" wa fedha za akaunti
ya escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2006. Akaunti hiyo
ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na Shirika la
Umeme Tanzania {TANESCO} kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Chimbuko la
akaunti hiyo ni mgogoro wa tozo hiyo kwamba iligubikwa na utata baada ya
kudaiwa kwamba Tanesco ilikuwa ikitozwa fedha nyingi kuliko inavyostahili.
Tuhuma za huo "wizi" hata hivyo
hazikuishia tu kwa wahusika wakuu yaani makampuni ya umeme, bali zimetiririshwa
hadi kwa watu binafsi ambao kimsingi hawana uhusiano wowote na mgogoro huo wa
malipo na wala kuhusika kwa njia yoyote na hicho kinachodaiwa kwamba ni uporaji
wa fedha za akaunti hiyo ya Escrow.
Akaunti Escrow ni akaunti ya amana ambayo
inawekwa chini ya uangalizi wa mtu wa tatu ili huyo mwangalizi aikabidhi kwa
mlengwa pale tu masharti kadhaa yatakapokuwa yamekamilishwa. Hivyo basi akaunti
hiyo maalum ya amana ilifunguliwa na kuwekwa chini ya Benki Kuu kama wakala
anayesubiria kutekelezwa kwa masharti maalumu ili aikabidhi kwa wenye kumiliki
fedha hizo watakapomaliza tofauti zao.
Ni vizuri kuliangalia suala hili la
akaunti maalum ya amana kwa namna ambayo itawafanya wale wenye kiu ya kutaka
kujua ukweli kukidhi hamu yao.
Fedha iliyokuwa ikiwekwa katika akaunti hiyo ni
tozo ya uwezo wa mitambo ya kufua umeme ambayo kampuni ya IPTL ilikuwa ikiitoza
Tanesco. Baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID)
kupunguza tozo ya IPTL kutoka USD 3.6million kila mwezi mpaka USD 2.6million
kila mwezi baadaye TANESCO ilishauriwa vibaya na wanasheria kwamba tozo hiyo
bado ni kubwa kuliko mkataba baina ya IPTL na TANESCO Mei 26, 1995 unavyo eleza.
Ubishani uliozuka kati ya mtoa huduma
ya umeme yaani IPTL na mtumia huduma ya umeme yaani Tanesco ndio uliosababisha
kufunguliwa kwa akaunti hiyo maalum ya amana yaani escrow account katika Benki
Kuu ya Tanzania {BoT} kama njia salama ya kutunza fedha hizo hadi mgogoro
utakapokuwa umetatuliwa.
Ni muhimu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba mtoa
huduma yaani IPTL hasitishi kufua umeme na mtumiaji wa umeme yaani Tanesco naye
hakosi umeme wa kuuza kwa walaji wake. Hiyo ni busara ya kibiashara. Fedha hizo
zililipwa katika akaunti hiyo maalum kutokana na hati za madai au ankara kutoka
kwa mtoa huduma na si vinginevyo.
Kitu kimoja kilichojitokeza wazi ni
kwamba suala la akaunti hiyo maalum limekuwa likibeba sura mpya kila kukicha na
la kusikitisha zaidi ni kwamba vyombo vya habari vilivyo vingi ama vimekuwa
vikipotosha kwa makusudi au kwa kutokuelewa mada yenyewe ipasavyo. Vipo vyombo
vya habari kwa mfano ambavyo vimedai kwamba "Benki ya Standard Chartered
ndiyo mmiliki wa mitambo ya IPTL baada ya kupewa mamlaka hayo na mahakama -
Deed of Assignment- inayoiruhusu kuchukua na kumiliki mali za IPTL kutokana na
kushindwa kulipa mkopo.
Aidha
kwa mujibu wa gazeti la Mawio la Alhamisi Novemba 20-26, 2014 mkataba huo
uliipatia benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na
kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Mawio
Benki ya Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama
deni linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani
138 milioni zinazotokana na mkopo pamoja na riba. Kwa mujibu wa uchambuzi wa
Mawio madai hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa gazeti hilo "nyaraka za
serikali zinaonesha kuwa PAP iliamuriwa kulipa wadai wote wa IPTL lakini haikuilipa
Benki ya Standard Charted ambayo inajitangaza kuwa ni moja ya wadai.
Ni vyema na busara kuanza uchambuzi
huu kwa kufanya nukuu hiyo muhimu sana kutoka katika gazeti la kila wiki la
Mawio kwa sababu inatusaidia kuonyesha waziwazi kwamba hiki kinachodaiwa kwamba
ni kashfa ya fedha za Escrow kina sura nyingi sana kulingana na maslahi
yanayolengwa kutetewa.
Katika muktadha huu ni wazi kwamba anayetetewa hapa ni
Benki ya Standard Chartered ambayo inadaiwa kwamba ndiyo yenye haki ya kulipwa
fedha kutoka katika akaunti ya Escrow na kwa mantiki hiyo imeishitaki Serikali
ya Tanzania katika Mahakama ya Uingereza.
Deni linalodaiwa kwamba Tanesco
inadaiwa na Standard Chartered la dola za Marekani linatokana na gharama za
umeme uliozalishwa na IPTL na nyingine ni mkopo na riba. Inashangaza kwamba
Tanesco inawezaje kudaiwa na Benki ya Standard Chartered wakati aliyezalisha
umeme ni IPTL? Abrakadabra hiyo ndiyo inayomfanya ye yote yule mwenye akili
timamu kutambua kwamba kuna mchezo wa kiini macho unaochezwa na benki hiyo
dhidi ya Tanzania.
Ni wazi kabisa kwamba benki hiyo
inalazimisha kuwapo na mgogoro wa kuhusu akaunti ya Escrow kwa lengo moja tu
nalo ni kuhakikisha kwamba wanapata nafasi ya kukwapua hizo fedha wanazodai
kwamba sio halali kuchukuliwa na IPTL. Kwamba zikichukuliwa na Benki ya
Standard Chartered ambayo haijazalisha umeme wala kuwa na ushahidi wowote wa
kushiriki katika kuzalisha umeme ni halali kabisa na zikichukuliwa na IPTL
ambayo imezalisha umeme na inayo mikataba ya kuuziana umeme na Tanesco si
sahihi, ni wizi, ni ujambazi ni hila na kashfa. Hii inahitaji maelezo zaidi
kushinda haya yanayotolewa hivi sasa.
Ukweli wa mambo ni kwamba mazungumzo
kuhusu fedha za Escrow na hususan habari za kujaribu kuonyesha kwamba umiliki
wake ni batili una lengo moja tu nalo ni kuandaa mazingira kwa ajili ya Benki
ya Standard Chartered hatimaye kuzichukua fedha hizo kwa kutumia kigezo cha
kwamba imemilikishwa mitambo ya IPTL na kwamba ndiyo iliyokuwa na haki ya kulipwa
tozo ya uzalishaji umeme na si kampuni nyingine yoyote. Hivyo ndivyo kampuni
hiyo inavyodai katika kesi iliyofungua dhidi ya Serikali ya Tanzania huko
Uingereza.
Benki ya Standard Chartered inatumia
mbinu mbalimbali ili kuhakikisha inafikia lengo lake la kukwapua fedha za
kigeni si chini ya dola milioni 200 kutoka kwa serikali ya Tanzania. Moja ya
njia inayotumia ni propaganda ambayo hupenyezwa katika vyombo vya habari kwa
kutumia majukwaa mbalimbali.
Moja ya njia zinazotumika ni kujaribu kuufanya umma
uamini kwamba fedha zilizotoka katika ufungaji wa akaunti hiyo ya Escrow
zimeibwa na kwamba wahusika katika huo wizi ni pamoja na viongozi kadhaa wa
Serikali.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba
kuhusishwa kwa watu hao kunafanyika bila hata ya kuwataka wajieleze kama
wanaelewa kile wanachotuhumiwa nacho. Wafadhili wa propaganda hizo hawakubali
kujitokeza hadharani moja kwa moja kwa kuhofia kuumbuliwa. Matukio huchukuliwa
si kwa ujumla wake bali upande mmoja na kuyatangaza kwa namna ya kukidhi
matakwa na matarajio yao tu.
Tumezoea kuambiwa kwamba wakati suala
linapokuwa mahakamani kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi basi si sahihi kuendelea
kulijadili kwenye vyombo vya habari kwani kwa kufanya hivyo ni sawa kabisa na
kuingilia uhuru wa mahakama. Ni wazi kwamba hata suala linapokuwa katika
uchunguzi au upelelezi uwe kwa kutumia tume maalum au makachero basi ni muhali
kulizungumzia hadharani na kuwatuhumu na hata kuwahukumu watu kwa ujasiri usio
na kikomo kwamba ni wezi au mafisadi au wakumbatiaji wa madhila hayo yote. Hili
linafanyika kila siku kupitia vyombo vya habari na chimbuko lake ni baadhi ya
wabunge na wanasiasa ambao hufanya hivyo huku wakitumia kila aina ya takwimu za
kweli na za kughushi au kubuni tu kichwani.
Nini kinachowafanya au kuwapa jeuri
hawa watu wanaowatuhumu na kuwahukumu wengine bila ya kujali kwamba hilo
halitakiwi wala kupaswa kufanyika bila ya kupitia katika vyombo vya sheria ili
kutoka fursa kwa wengine kujitetea? Swali hilo linastahili kujibiwa kwa umakini
mkubwa ili kubaini kama kweli hao wanaodai kwamba wanapigania haki ya kiuchumi
ya Watanzania ni kweli wanafanya hivyo kwa dhati ya moyo wao kabisa bila ya
kuwa na nia nyingine iliyojificha ambayo hawathubutu kuiweka hadharani kwani
kwa kufanya hivyo watageuka viroja.
Pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani dhidi
ya Serikali ya Tanzania ni wazi kwamba ukiwauliza Standard Chartered
kilichowapeleka mahakamani wanasema kwamba wanaionea nchi yetu huruma, Hata
hivyo, kamwe hakuna atayekuambia kwamba amekuja hapa kwa ajili ya kujaribu
bahati yake kama wanaweza kufanya mbinu wakatengeneza fedha ya bure. Ili
kufanikisha malengo yao tuhuma hurushwa kwa yeyote na popote. Ili kufanikisha
malengo hayo mtu yeyote yule aweza kuunganishwa katika lolote lile ili kufikia
lengo.
Ni kwa utaratibu huo huo ndio
tunashuhudia jinsi jitihada za Profesa Anna Tibaijuka za kuendeleza mtoto wa
kike kielimu zinavyopakwa matope na kukejeliwa mno kwa sababu tu ameomba msaada
mahali na akaupata.
Tujiulize inakuwaje wanasiasa wetu wanathubutu kumhukumu
Profesa Tibaijuka na kumuita kila aina ya majina machafu. Ametuhumiwa kwamba ni
mwizi eti kwa sababu aliomba msaada kwa ajili ya shule ya Babro Johansson
ambayo ni kwa madhumuni ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu.
Profesa
Tibaijuka aliomba msaada kwa barua rasmi miaka kadhaa iliyopita na kampuni hiyo
haikuweza kumsaidia mapema kutokana na ukata na ni hivi majuzi hali ilipokuwa
njema ndipo ikatoa msaada huo.
La kustaajabisha ni kwamba msaada huo
haukuwa ni siri na ulitolewa kwa uwazi mkubwa bila ya kificho. Sasa huo ujambazi
wa Profesa Tibaijuka umetokea wapi? Kosa lake ni kupatiwa fedha alizoomba kwa
ajili ya kuisaidia shule ambayo aliianzisha?
Tunajiuliza hapa, baada ya VIP kuuza hisa zake kwa PAP na
kulipwa na PAP stahili yake, ilifanya kosa gani kutoa msaada kwa shule ya Babro
Johansson?
Mahitaji na umuhimu wa elimu yanajulikana. Viongozi wanahimiza
kila leo umuhimu wa Watanzania kubadilika kuchangia Maendeleo ya Elimu badala
ya harusi na sherehe nyinginezo. Leo hii anatokea Mtanzania anaomba msaada wa
kuendeleza elimu na anapatikana Mtanzania anakubali kuchangia vizuri maendeleo
ya elimu, wawili hawa baadhi ya wanaojiita viongozi wa siasa tena wenye kutaka
kuchukua madaraka ya juu kuiongoza nchi, wanalalamika na hata kutamani kutoa
roho ya mtu! Watanzania tuzipime dhamira zao. Ni wadanganyifu wasio na uelewa
halisi wa matatizo na vipaumbele vya taifa na hivyo kukosa dhamira thabiti ya
kuyashughulikia. Wanasukumwa zaidi na tamaa zao binafsi.
Kwa wanaong'ang'ania kudai damu za baadhi ya watu
kutokana na hukumu ambayo wao wameipitisha baada ya kufanya kila kitu wao ikiwa
ni pamoja na kutuhumu, kupeleleza, kufungua mashitaka, kusikiliza kesi na
hatimaye kuhukumu na sasa kutaka kukaza hukumu kwa njia yoyote ile hakuna jambo
zuri na jema kama kufanya kile wanachotaka wao yaani kukubali kwamba fedha zote
katika akaunti maalum ya escrow ni za serikali na kwamba lazima zirudi
serikalini.
Hata hivyo, wakubwa hao hawataki kurudi nyuma na kujiuliza ni kwa
njia gani fedha hizo zimeingia katika akaunti hiyo. Aidha, hawataki kujiuliza
kwamba kama Tanesco ndio ilikuwa ikitumbukiza fedha katika akaunti hiyo,
ilikuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vigezo gani. Swali linguine la kujiuliza, je
Serikali hutunza pesa zake kwenye Account zake Benki Kuu au kwenye Escrow
Account?
Hawaoni mantiki ya kutulia na kujibu
swali la msingi kwamba kama Tanesco ingelikuwa inatumbukiza fedha katika
akaunti hiyo kwa ajili ya kugharamia tozo la uwezo wa mitambo kuzalisha
umeme sasa inakuwaje fedha hizo zirudi tena Tanesco? Ni maswali ambayo
wanaojiamini kwamba ukweli wanao wao tu hawataki kuyajibu hata kidogo kwani kwa
kufanya hivyo watakuwa wanaumaliza utamu wa mchezo wao wa kuigiza.
Fedha hizo
zinatakiwa zirudi Tanesco ili Benki ya Standard Chartered izichukue kwa madai
kwamba ndiye mmiliki halali wa IPTL na kwamba kuna deni kama ilivyoainishwa
awali katika makala haya.
Kutokana na ufafanuzi huo hapo juu ni
wazi basi kwamba Tanesco ilikuwa ikilipia gharama za huduma ambayo ilikuwa inaipata
kutoka kwa IPTL. Hilo halina ubishi.
Lakini pia
suala lingine ambalo sasa halina ubishi japo halisemwi makusudi kwa sababu za
upotoshaji ni kwamba katika makampuni yote ambayo yanauzia umeme TANESCO, IPTL
ndiyo kampuni pekee inayotoza kiwango kidogo cha malipo ya uwekezaji (capacity
charges). Suala la kujiuliza hapa ni inawezekanaje IPTL ambayo inatoza kiwango
kidogo cha capacity charges ionekane “kuiibia” Serikali kwa kulipwa halali yake
wakati makampuni mengine yanatoza capacity charges kwa kiwango cha juu zaidi ya
IPTL na hakuna malalamiko.
Swali
la kujiuliza ni kwamba ni kitu gani kinachowasukuma watuhumu kutafuta kila njia
ya kuonyesha kwamba kuna hitilafu kubwa sana kwa namna ambavyo suala la akaunti
hiyo lilivyohitimishwa?
Ukifuatilia kwa karibu na umakini
jinsi ambavyo tuhuma zimekuwa zikitolewa ni kwamba kinacholengwa ni fedha
zilizokuwa katika akaunti maalumu ambazo ni tozo ya uwezo wa ufuaji wa umeme.
Fedha hizo zinagombewa na Benki ya Standard Chartered ambayo ina matawi yake
hapa nchini.
Benki hiyo inatumia kila njia kujaribu kuonesha kwamba fedha
zilizokuwapo katika akaunti ya Escrow ni fedha ya Serikali. Kwa mantiki hiyo
inachojaribu kufanya Benki hiyo ni kuonyesha kwamba fedha akaunti ya escrow si
kwa ajili ya kulipia gharama za uwezo wa mitambo kufua umeme la hasha. Bali ni
fedha za Tanesco na kamwe hakuna anayestahili kuzipunguza kwa njia yoyote ile.
Cha
kushangaza, hata hivyo, ni kwamba benki hiyo, inayodai kuwa iliikopesha fedha
IPTL, katika madai yake yaliyopo mahakamani, inadai kuwa yenyewe ndiyo
ilistahili kupata fedha zilizokuwa kwenye escrow account! Swali hapa ni je,
hiyo asasi ndiyo Serikali? Je, fedha zilizokuwa kwenye escrow account zinakuwa
za Serikali na siyo IPTL kwa sababu benki hiyo haijalipwa?
Jitihada za kutaka kuhalalisha kwamba fedha hizo ni
mali ya Tanesco na kwamba haziwezi kumegwa hata kidogo zinafanywa na Benki ya
Standard Chartered ambayo inataka kutengeneza mazingira ya kuchota fedha kutoka
Tanesco kwa madai kwamba ndiyo inayostahili kuwa mlipwaji wa fedha hizo
kutokana na deni ambalo kwa mujibu wa madai yao ndio walioikopesha IPTL fedha
kwa ajili ya mradi huo wa umeme.
Mchezo ambao benki hiyo inafanya hapa
nchini ni kuhakikisha kwamba vyombo vya habari vinaandika habari za kuigonganisha
serikali na wananchi kwamba Serikali ni ya mafisadi na inayokumbatia ufisadi,
na haina ubavu wowote wa kupambana na rushwa. Aidha, asasi hiyo imevirubuni
baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari kwamba Mahakama za Tanzania
haziaminiki na zinakumbatia ufisadi na kwamba zimekubuhu kwa rushwa.
Cha
kushangaza, tuhuma hizi za rushwa kwa Mahakama za Tanzania zinakuja muda mfupi
tu baada ya benki ya Standard Chartered kuiambia mahakama New York, nchini
Marekani iliposhitakiwa na VIP kuwa Mahakama za Tanzania ndizo zenye uwezo wa
kusikiliza na kutatua migogoro ya IPTL.
Mchezo ambao
Standard Chartered Bank inaufanya ni kutumia vyombo vya habari kutoa habari
zisizo za kweli na za upotoshi ili kuwachochea watu dhidi ya Serikali yao
kutokana na nini kinaendelea ndani ya IPTL.
Mambo mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusiana na Mahakama na watendaji wa
Serikali kula rushwa. Madhumuni ya
kufanya hivyo ni kutaka kuonyesha kwamba nchini Tanzania haki haiwezi
kutendeka.
Madai hayo yote,
yanatokea wakati Standard Chartered Bank imefungua kesi London, kwa kisingizio
kwamba Mahakama za Tanzania haziwezi kutenda haki
Kwa vipi Standard
Chartered Bank inatoa madai kulipwa dola za kimarekani 208 milioni kutoka
TANESCO (katika kesi ilivyofunguliwa Mahakama ya usuluhishi (ICSID)) kwa mkopo
wa dola milioni 84 kwa IPTL, wakati Serikali ya Tanzania na TANESCO tayari
walikwishalipa takribani dola 200 milioni kwa IPTL kufikia mwaka 2006. Kiasi hicho kingelitosha kulipia mkopo uliokuwa
umechukuliwa na kulipa gawiwo kwa VIP na MECHMAR. Mpaka mwaka 2013 VIP ilikuwa haijalipwa hata senti
moja kwa jina lolote.
Kampuni ya
Mechmar ilitumia fedha zilizodaiwa na IPTL kutoka Serikali ya Tanzania na
TANESCO kwa kujilipa yenyewe na Kampuni ya Wartsila madeni hewa (kwa
makubaliano na benki ya Danaharta na baadaye Standard Chartered Bank (Hong
Kong) Ltd.
Standard
Chartered Bank (Hong Kong) Ltd inajaribu kutekeleza mpango haramu dhidi ya IPTL
kwa kutumia dhamana ya Serikali ya Tanzania na hivyo Serikali ina sababu za
kutaka Standard Chartered Bank ithibitishe kama inaidai IPTL.
Mpaka sasa ukweli
ni kwamba Standard Chartered Bank imekwepa kutoa ushahidi kuwa ina madai yoyote
dhidi ya IPTL na kwa sababu hiyo na zingine VIP na IPTL/PAP wameifungulia kesi
za madai ya fidia na hasara ya TZS 787bilioni na USD 3bilioni katika Mahakama
Kuu ya Tanzania. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)
No comments:
Post a Comment