Mkuu wa wilaya ya Iringa Dr Leticia Warioba ( waliokaa katikati) akiwa na naibu kamishina wa madini kanda ya Mbeya Wilfred Machumu na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu kushoto katika picha ya pamoja na wachimbaji wa madini wadogo mkoa wa Iringa na Njombe mara baada ya kufungua mafunzo ya madini ya siku tatu Veta mjini Iringa
WACHIMBAJI wadogo wa madini mkoani Iringa wamempongeza Waziri wa Nishati na Madini Profesa
Sospeter Muhongo kwa kuendelea kuisuka upya wizara yake kwa
kuwaondoa watendaji waliokuwa wakifanya kazi kwa misingi ya
ubabaishaji mkubwa katika ofisi za umma na kutaka kuendelea
kuwaondoa wale wote watakaobainika kuendekeza rushwa wakati wa
utoaji wa vibali .
Wataka
waziri Prof Muhongo kuwatimua kazi watumishi wake wasio
waaminifu ambao wameendelea kuchochea migogoro kwa kuwakumbatia
wachimbaji wakubwa na kuwaacha wadogo .
Alisema
kuwa mbali ya wachimbaji hao wadogo kukabiliwa na mitaji katika
kuifanya kazi hiyo ila bado ofisi ya kamishina wa madini mikoa ya
kusini ilikuwa ikiwajali zaidi wachimbaji wakubwa na hata
kuwanyima vibali wachimbaji wadogo hali ambayo kwa sasa imetoweka
na kubaki tatizo la mitaji kwa wachimbaji hao wadogo .
Hata
hivyo alisema kuwa mara zote maeneo ambayo wanapewa vibali
wachimbaji wakubwa ni maeneo ambayo yamegunduliwa na wachimbaji
wadogo na kupitia uwezo wao wa kifedha wachimbaji hao wakubwa
wamekuwa wakipewa maeneo yaliyogunduliwa na wachimbaji wadogo.
Kuhusu
migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa alisema kuwa
migogoro hiyo imekuwa ikichangiwa na baadhi ya watumishi wa wizara
ya Nishati na madini ambao si waaminifu ambao wamekuwa wakipokea
rushwa kutoka kwa wachimbaji wakubwa kwa kutumia nafasi yao ya
utoaji leseni ikiwa ni pamoja na kutoa kwa upendeleo kwa wenye fedha
pekee.
Pia
walipendekeza wizara hiyo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya
wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na kuwapokonya maeneo
wachimbaji wakubwa ambao wameshikilia maeneo makubwa huku
wachimbaji wadogo wakiendelea kukosa maeneo ya kuchimba madini huku
maeneo hayo makubwa yakiwa yamehodhiwa bila kuchimbwa .
Mwakilishi
wa ofisi ya madini kanda ya Mbeya Wilfred Machumu alisema kuwa
ofisi yake imeandaa mafunzo hayo kwa wachimbaji hao wadogo ili
kuweza kuwapa mwanga wa elimu ya madini na jinsi ya kuifanya kazi hiyo
kwa ubora zaidi.
Hata
hivyo alisema katika kupunguza malalamiko ya kukosa leseni alisema
kwa sasa wapo mbioni kuanzisha utaratibu wa kutumia maombi kwa njia
ya mtandao ili kukomesha rushwa na malalamiko katika sekta hiyo.
Pia
alisema katika kuwafanya wachimbaji hao kuboresha huduma zao
watawapa elimu ya kuomba mikopo kupitia benki na mkopo ambao
wataweza kupata ni kuanzia dola 30,000 kwa mchimbaji.
Kwa
upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Christine Ishengoma
aliyewakilishwa na mkuu wa wilaya ya Iringa Dr Leticia Warioba
alisema kuwa Serikali iliamua kutunga Sera mpya ya Madini ya Mwaka 2009
yenye kulenga kuimarisha fungamanisho la sekta ya madini na sekta
nyingine za uchumi
Pia
kuboresha mazingira ya kiuchumi ya uwekezaji kuongeza manufaa ya sekta
ya madini pamoja na kuboresha mazingira ya kisheria kwa lengo la
kuimarisha uwezo wa Serikali kusimamia sekta ya madini nchini.
"
kuwaendeleza wachimbaji wadogo kuhamasisha na kuwezesha uongezaji
thamani madini nchini...; na kuimarisha usimamizi wa mazingira"
Pamoja
na malengo hayo alisema kuwa Serikali itaendelea kuwa msimamizi
mwezeshaji na mhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya
madini, lakini tofauti na ilivyokuwa huko nyuma (Sera ya madini ya
mwaka 1997) kwa sasa Serikali itashiriki kimkakati katika miradi ya
madini kwa kupata hisa katika miradi hiyo.
" Naomba nianze kwa kusema kuwa Uchimbaji
mdogo kwa muda mrefu umekuwa ukitoa mchango wa uchumi katika Pato la
Taifa kwa kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania pamoja na kupunguza
kasi ya vijana kutoka vijijini kuhamia mjini"
Hata
hivyo, mchango wa sekta hii umekuwa ni mdogo kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo vifaa duni wanavyovitumia wachimbaji; ukosefu wa
maarifa na ujuzi, na ukosefu wa mtaji na teknolojia
HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA, MHE.
DKT. CHRISTINE ISHENGOMA WAKATI WA KUFUNGUA
MAFUNZO YA WACHIMBAJI WADOGO WA MKOA WA IRINGA TAREHE 16 - 18 JULAI,
2014
Mhe. Mkuu
wa Wilaya ya Iringa,
Mhe.
Mbunge wa Iringa
Kamishna
Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini
Magharibi
Viongozi wa
Wilaya ya Iringa,
Maafisa
kutoka Wizara ya Nishati na Madini,na taasisi zake,
Watendaji
wa Kata na Vijiji mlioko hapa,
Wachimbaji
wa madini waalikwa,
Waandishi
wa Habari,
Mabibi na
Mabwana.
Awali ya yote, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa
Wizara ya Nishati na Madini kwa kunipa nafasi hii ya kuwa Mgeni Rasmi katika
uzinduzi wa mafunzo ya kuwaelimisha wachimbaji wadogo wa madini wa Mkoa wa Iringa
na baadhi ya viongozi wa Mkoa huu kuhusu
usimamizi wa sekta ya madini. Nitumie
fursa hii kuushukuru uongozi wa Wizara hasa ofisi ya Madini Kanda ya Kusini
Magharibi kwa kuandaa mafunzo haya na kuyaleta katika Mkoa huu, hususan katika
kipindi hiki ambacho shughuli za uchimbaji madini nchini zinakabiliwa na
changamoto mbalimbali. Niwashukuru pia kwa kuacha shughuli zenu
ambazo ni muhimu kwenu na kukubali kuja kushiriki kwenye mafunzo haya muhimu.
Ndugu
washiriki wa Mafunzo, Kabla ya kufanya kilichotuleta hapa,
naomba nianze kwa kusema maneno machache kuhusu sekta ya madini.
Ndugu
washiriki wa Mafunzo, kama wengi wetu tunavyojua kuwa
Tanzania imejaaliwa kuwa na hazina ya madini ya aina mbalimbali ikiwemo madini
ya metali kama dhahabu na chuma; madini
ya vito vya thamani kama almasi na
tanzanite; madini ya viwandani; madini
ya ujenzi kama kokoto na mchanga; na madini ya nishati kama makaa ya mawe na
urani. Kufuatia uwepo wa hazina kubwa ya madini, na kufuatia marekebisho ya
kiuchumi yaliyofanywa katika miaka ya 1990, sekta ya madini nayo ilifanyiwa
marekebisho ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa Sera ya Madini mwaka 1997 na Sheria
ya Madini ya mwaka 1998.
Ndugu
washiriki wa Mafunzo, marekebisho hayo katika sekta ya
madini yalivutia kampuni nyingi za uwekezaji katika utafutaji, uchimbaji na
kukuza biashara ya madini nchini, hivyo kwa kipindi cha kati mwaka 1997 hadi
2007 mafanikio mbalimbali yaliyopatikana ikiwemo, kuanzishwa kwa migodi mikubwa
sita ya dhahabu ambayo ilizalisha wastani wa tani 50; kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya madini nje
ya nchi kutoka dola za Marekani milioni 26.66 hadi milioni 1,003.21; kuongezeka
kwa ajira kutoka wafanyakazi 1,700 hadi
13,000; na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la
Taifa kutoka asilimia 1.4 hadi asilimia 2.7 (kwa bei za mwaka 2001); na kukua
kwa sekta ya madini kutoka 7.7% hadi 10.7%
Ndugu
washiriki wa Mafunzo, pamoja na mafanikio yaliyopatikana,
sekta iliendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan, kiwango kidogo
cha fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi; mchango mdogo
katika Pato la Taifa ikilinganishwa na ukuaji wa sekta; kasi ndogo ya uendelezaji
wa uchimbaji mdogo; uwezo mdogo wa Serikali kusimamia sekta ya madini; kiwango
kidogo cha uongezaji thamani madini; na uharibifu wa mazingira.
Ndugu
washiriki wa Mafunzo, kufuatia changamoto hizo, Serikali
iliamua kutunga Sera mpya ya Madini ya Mwaka 2009 yenye kulenga: kuimarisha
fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi; kuboresha
mazingira ya kiuchumi ya uwekezaji; kuongeza manufaa ya sekta ya madini;
kuboresha mazingira ya kisheria; kuimarisha uwezo wa Serikali kusimamia sekta
ya madini; kuwaendeleza wachimbaji wadogo; kuhamasisha na kuwezesha uongezaji
thamani madini nchini; na kuimarisha usimamizi wa mazingira. Pamoja na malengo
hayo, Serikali itaendelea kuwa msimamizi; mwezeshaji; na mhamasishaji wa
uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya madini, lakini tofauti na ilivyokuwa
huko nyuma (Sera ya madini ya mwaka 1997) kwa sasa Serikali itashiriki
kimkakati katika miradi ya madini kwa kupata hisa katika miradi hiyo.
Ndugu washiriki wa Mafunzo, Kuhusu kilichotuleta hapa leo hii, Naomba nianze kwa kusema kuwa Uchimbaji
mdogo kwa muda mrefu umekuwa ukitoa mchango wa uchumi katika Pato la Taifa kwa kuongeza ajira na kipato
kwa Watanzania pamoja na kupunguza kasi ya vijana kutoka vijijini kuhamia
mjini. Hata hivyo, mchango wa sekta hii
umekuwa ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifaa duni
wanavyovitumia wachimbaji; ukosefu wa maarifa na ujuzi, na ukosefu wa mtaji na
teknolojia. Sera ya Madini ya Tanzania inatambua umuhimu na mchango wa
uchimbaji mdogo wa madini katika kuinua uchumi.
Ndugu washiriki wa Mafunzo, kufuatia
umuhimu huo mwaka 2006, Wizara ya Nishati na Madini iliandaa mikakati ya
kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini sambamba na malengo ya MKUKUTA. Pamoja na
malengo mengine, mikakati hiyo ya kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini imelenga
kurahisisha upatikanaji wa vifaa na nyenzo za uchimbaji, kukuza na kuboresha
shughuli za uongezaji thamani madini na pia kusaidia vikundi vya wanawake wachimbaji.
Aidha,
Kwa kutambua mchango wa uchimbaji mdogo katika Pato la Taifa, na kwa kutambua
changamoto walizonazo wachimbaji wadogo, Serikali imefanya juhudi za kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini
nchini kwa kuwapatia ujuzi na maarifa kwenye nyanja za uchimbaji, uchenjuaji na
uongezaji thamani madini; na kuwapatia maeneo ya uchimbaji. Aidha, Serikali
imeanzisha Mfuko wa Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo. Katika Semina hii
mtafahamishwa fursa zilizopo kupitia mfuko huu.
Ndugu washiriki wa Mafunzo, nimejulishwa kuwa katika mafunzo haya mtapata uelewa na
fursa ya kujadili mada zifuatazo: Sera
ya madini, 2009 na Sheria ya Madini ya Mwaka, 2010 na Kanuni zake; Utaratibu wa
kupata na kumiliki leseni ndogo za uchimbaji madini na biashara ya madini;
Wajibu na Majukumu ya wakala wa ukaguzi wa madini Tanzania, yaani Tanzania
Mineral Audit Agency (TMAA); Matumizi ya Hati ya Mauzo ya Madini katika
Kusimamia Uzalishaji na Uuzaji madini; Utafutaji na Uchimbaji Salama wa Madini
Migodini; Utunzaji wa Mazingira Migodini; Utaratibu wa Upatikanaji, Kumiliki na
Utumiaji wa Baruti Katika Uchimbaji Madini; Mafunzo ya Biashara na Ujasiriamali
katika shughuli za Madini; Maelezo juu ya Mfuko wa Kuendeleza Uchimbaji Mdogo
wa Madini; na Masuala MTAMBUKA (Jinsia, Ajira kwa watoto & Ukimwi)
Ndugu washiriki wa Mafunzo, katika mafunzo haya, mtaelimishwa jinsi Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania unavyosimamia shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini na
jinsi unavyotarajia kuanzisha utaratibu wa kuweka vocha za uzalishaji na
biashara ya madini. Shughuli
zinazofanywa na Shirika la madini nchini (STAMICO), ikiwemo masoko. Ninawasihi
kusikiliza kwa makini Mada hizo na kushauri ipasavyo ili kazi hiyo iweze
kufanyika kwa ufanisi zaidi. Ni matarajio yangu kuwa baada ya kupata uelewa huo,
kila mmoja atapata fursa ya kutoa elimu hiyo kwa wananchi tunaowaongoza kwa upande wa viongozi
na wachimbaji kuitoa elimu hiyo kwa wale wanaofanya kazi chini yenu au wachimbaji wengine ambao hawakupata bahati
ya kuhudhuria mafunzo haya.
Ndugu washiriki wa Mafunzo, ni muhimu kila mmoja wetu kuijua kwa ufasaha Sheria Mpya ya Madini ambayo
inatumika katika kuongoza na kusimamia sekta ya madini. Ninatambua kuwa sekta
ya madini inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na: (1) leseni za
uchimbaji mdogo wa madini kutotolewa kwa wakati; (2)
ukosefu wa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo; (3) suala la fidia ili
kupisha, shughuli za migodi, na (4) uharibifu wa mazingira unaosababishwa na
shughuli za utafiti na uchimbaji madini. Hivyo, kama watendaji na wasimamizi wa
wananchi katika Mkoa huu, ni muhimu kujua vipengele vya sheria vinavyohusika katika
kukabiliana na changamoto hizo na kuhakikisha tunazitumia kwa kushirikiana na
Maafisa wa Madini ili kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa maeneo
yetu. Hivyo, ni matumaini yangu kuwa mtasikiliza na kuchangia Mada hizo kwa
umakini mkubwa.
Ndugu washiriki wa Mafunzo, naomba nihitimishe Hotuba yangu kwa kuipongeza sana Wizara ya Nishati na
Madini kwa kuandaa mafunzo haya na kuyaleta hapa Iringa. Ni matarajio yangu
kuwa elimu tutakayoipata hapa na ushauri tutakaoutoa kwa Wizara husika
utasaidia sana katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini kwa manufaa ya
Taifa. Hivyo, niwaombe wote kutumia nafasi hii kujadiliana kwa mtazamo chanya ili
kwa pamoja tuhakikishe kwamba sekta ya madini inatoa mchango unaostahili kwenye
uchumi.
Baada ya kusema hayo, napenda sasa kutamka kuwa mafunzo haya yamefunguliwa RASMI.
ASANTENI
SANA KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment