Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Ada za uhakiki wa filamu hapa nchini zipo kwa
mujibu wa sheria na kanuni, ambapo gharama hizo hulipwa kwa nakala mama
na baada ya hapo mtayarishaji huzalisha nakala kwa idadi anayohitaji.
Naibu
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Anastazia Wambura ameyasema
hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa
Mafinga Mjini Cosato Chumi juu ya Serikali ina mpango gani wa
kuwapunguzia wasanii gharama za ukaguzi ambapo kwa hivi sasa gharama
hizo ni shilingi elfu moja kwa dakika.
“Nchi
yetu hutoza ada ambazo ni rafiki ukilinganisha na nchi nyingine, kwa
mfano, Nigeria ambayo ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwa upande wa
filamu, hutoza filamu yenye urefu wa dakika 60 (filamu ya lugha asili)
Naira 30,000 sawa na zaidi ya dola 150 ambayo ni sawa na Sh. 337,950 za
Kitanzania na Kenya, ni sawa na Sh. 190,000,” alifafanua Anastazia
Wambura.
Aliendelea
kwa kusema kuwa Tanzania hutoza filamu za Kitanzania zenye urefu wa
dakika 60 kwa Sh. 60,000 (sawa na Sh. 1,000 kwa dakika) ambapo gharama
hizo ni sawa na asilimia 18 ya gharama za Nigeria na asilimia 32 ya
Kenya.
Hivyo
basi Tanzania imekuwa ikitoza ada hiyo ya uhakiki wa filamu kwa gharama
nafuu na rafiki ukilinganisha na nchi nyingine Afrika.Akijibu
swali la namna gani Bodi hiyo imejipanga kuhakikisha huduma zao
zinatambulika nchi nzima tofauti na sasa ambapo wasanii wachache ndiyo
wanafahamu wajibu na majukumu ya Bodi hiyo, Wambura amesema kwamba Bodi
hiyo imeendelea kujitangaza kwa wadau kupitia shughuli mbalimbali za
kitaifa na Kimataifa kama vile kushiriki katika maonesho ya Sabasaba.
Vile
vile bodi hiyo imekuwa ikishiriki katika wiki ya Vijana na Kilele cha
Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni
Festivals (JAMAFEST). Pia hutumia vyombo mbalimbali vya habari kama vile
TBC1, E-FM, Clouds media pamoja na magazeti mbalimbali kueleza
watanzania kazi zinazofanywa na Bodi hiyo.
Aidha
Bodi hiyo imekuwa ikifanya warsha za kuwajengea wadau wake weledi katika
masuala ya filamu sehemu mbalimbali ikiwemo mikoani na wilayani ikiwa
ni moja ya maeneo ya kujitangaza.
No comments:
Post a Comment