Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa India nchini Mhe. Sandeep Arya (kushoto) aliyemtembelea Makamu wa Rais ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Sudan nchini Mahgoub A. Sharfi (kushoto) alimtembelea na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.
...............................................................................
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na India ambayo yamedumu kwa muda mrefu hasa katika sekta mbalimbali ikiwemo za elimu,afya na biashara.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo 25-Okt-2016 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Sandeep Arya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema mahusiano kati ya Tanzania na India yamesaidia kunufaisha wananchi wa nchini mbili hasa katika masuala ya kibiashara,miradi ya maendeleo na hivyo mahusiano hayo ni muhimu yakaendelezwa na kudumishwa.
Makamu wa Rais katika mazungumzo na balozi huyo wa India hapa nchini Sandeep Arya pia ameiomba serikali kuisaidia Tanzania katika mpango utakaosaidia wakulima kupata taarifa mbalimbali zinazohusu kilimo na masoko ya bidhaa zao kupitia simu za mkononi ili kuondoa usumbufu mkubwa wanaopata wakulima kwa sasa hasa kuhusu masoko.
Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Tanzania Sandeep Arya amemhakikishia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan serikali yake itakuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha wananchi wa pande Mbili wananufaika na mahusiano yaliyopo.
Balozi Sandeep Arya amesisitiza kuwa serikali ya India itaendelea kuisaidia Tanzania katika uimarishaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na miradi ya maendeleo na uimarishaji wa shughuli za kiuchumi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sudan nchini Tanzania Mahgoub Sharfi mazungumzo yaliyolenga pamoja na mambo mengine kuhusu namna ya kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Sudan.
No comments:
Post a Comment