Serikali ya Wilaya Magharibi B
imetoa muda wa siku mbili kwa wauza samaki pembezoni mwa soko kuu la
Mwanakwerekwe kuondoka na atakaepuuza agizo hilo atachukuliwa hatua za
kisheria.
Akizungumza na wauza samaki hao
Ofisini kwake Mwanakwerekwe, Mkuu wa wilaya Magharibi B Silima Haji
Haji amesema Serikali imekuwa ikichukuwa juhudi mbali mbali za
kuwaelekeza sehemu zinazostahiki za kufanya biashara hiyo lakini
wamekuwa wakikaidi agizo hilo na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa
Barabara.
Amesema kabla ya kutoa msimamo
huo serikali ya Wilaya imekaa na wauza samaki hao mara kadhaa na
kukubaliana kuondoka lakini lakusikitisha wamekuwa wakiondoka kwa muda
na baadae kurejea tena katika eneo hilo.
Amefafanua kuwa uuzaji wa samaki
katika eneo la nje ya soko la Mwanakwerekwe kunasababisha uchafu
kutokana na matumbo ya samaki, vumba na kutapakaa Damu katika eneo hilo
jambo ambalo limekuwa likiondosha haiba ya soko.
Aidha Mkuu wa Wilaya ameutaka
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Magharibi B kufuatilia agizo hilo
haraka iwezekanavyo ikiwemo kuwachukulia hatua wale watakaokadi agizo
hilo.
Akizungumza katika kikao hicho,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Magharibi B Amour Ali Mussa amesema
sababu ya kuongezeka tatizo hilo ni pamoja na kutokuwepo kuwepo
mipango mizuri ya mji wa Zanzibar inayoonyesha mgawanyo mzuri wa masoko
na mahitaji ya wateja.
Mkurugenzi Amour mesema wauza
samaki hao wametakiwa kuhamia soko la samaki Mikunguni lakini wamekuwa
wakipinga kwa madai hakuna biashara na wamekukwa wakikosa wateja.
Amesema Halmashauri kwa
kushirikiana na Wilaya inaandaa mipango maalum itakayoweza kutoa mvuto
kwa wananchi wengi kuenda kufuata huduma katika soko hilo la Mikunguni.
Amesema wanafanya utaratibu wa
kuweka kituo kikubwa cha daladala ili wananchi wengi waweze kufika na
kuhamisha Mnada wa Samaki soko la Darajani na kuhamia katika soko hilo.
Mapema wafanyabiashara hao wa
Samaki wamesema hawapingi kuhamia soko la Mikunguni lakini
kinachopelekea kubakia nje ya soko la Mwanakwerekwe ni kukosa wateja na
kupata hasara katika biashara yao.
Wamesema hawana tatizo kuondoka
sehemu ili kutii amri ya Serikali lakini wameiomba kuandaliwa mazingira
mazuri yatakayowawezesha kufanyabiashara itakayo waongezea kipato chao.
No comments:
Post a Comment