Mkuu
wa Polisi wilaya ya Arusha (SSP) Emmanuel Tille akiongea na viongozi wa
kata ya Moivaro tarafa ya Suye pamoja na askari wa vikundi vya ulinzi
shirikishi wakati wa uzinduzi wa vikundi vinne vya kata hiyo.
Diwani
wa kata ya Moivaro Rick Moiro akiongea na askari wa vikundi vya ulinzi
shirikishi toka kwenye baadhi ya mitaa ya kata yake mara baada ya
uzinduzi wa vikundi hivyo.
Mkuu
wa Polisi wilaya ya Arusha (SSP) Emmanuel Tille akiwakagua askari wa
vikundi vya ulinzi shirikishi kutoka mitaa ya Ngurumausi, Oldonyommasi,
Moivaro Kati na Shangarao. Baadhi
ya viongozi wa kata ya Moivaro pamoja na askari wa vikundi vipya vya
ulinzi shirikishi wakimsikiliza kwa umakini Mkuu wa Polisi wilaya ya
Arusha (SSP) Emmanuel Tille hayupo pichani.
Mmoja
wa wahitimu wa askari wa ulinzi shirikishi katika kata ya Moivaro
akikabidhiwa kitambulisho cha kazi kutoka kwa Mkuu wa Polisi wilaya ya
Arusha (SSP) Emmanuel Tille.
—————————
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Ikiwa jeshi la Polisi linaendeleza
harakati za kupambana na uhalifu ili kupunguza matukio ya namna hiyo,
wananchi wa kata ya Moivaro tarafa ya Suye halmashauri ya jiji la Arusha
hawapo mbali na jitihada hizo hivyo kuamua kujitokeza kwa moyo mmoja
kupinga uhalifu kwa kuanzisha vikundi vinne vya ulinzi shirikishi kutoka
mitaa ya Ngurumausi, Oldonyommasi, Moivaro Kati na Shangarao.
Akizindua vikundi hivyo ambavyo
vimewezeshwa na wadau walioongozwa na Jeff Mligha ambao walijitolea
vifaa mbalimbali vya ulinzi zikiwemo tochi, Mkuu wa Polisi wilaya ya
Arusha Mratibu Mwandamizi wa Polisi Emmanuel Tille kwa niaba ya Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha alisema kwamba matarajio ya wananchi katika
kata hiyo ya Moivaro ni makubwa na ana imani watakuwa wanalala na kuamka
salama hivyo kuwataka walinzi hao wawe na nidhamu kwenye kazi yao.
“Kazi ya ulinzi ina miiko yake;
kitu cha kwanza ni nidhamu ya hali ya juu. Mimi mwenyewe mpaka nafikia
hatua hii ni kwa sababu ya nidhamu na nawataka ninyi muige mfano wangu,
ninachosema hapa ni pamoja na kuwahi kazini, kutunza siri pasipo
kuwazunguka wenzako pamoja na kufuata maelekezo ya wakubwa wa vikundi
vyenu” Alisisitiza Tille.
Alisema japokuwa askari hao
wapatao 42 wamepewa mafunzo lakini kupitia Wakaguzi wa Polisi wa Tarafa
na askari kata wataendelea kuwapa mafunzo mara kwa mara ili waweze
kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, huku akiwaonya wasijichukulie
sheria mkononi.
Aliwataka wananchi wanapopata
taarifa watoe kwa viongozi wa Polisi mara moja ili ziweze kufanyiwa kazi
kwa haraka na hatimaye kufikia malengo ya kupunguza uhalifu ndani ya
jiji la Arusha, huku akiwataka watendaji wa kata na Wakaguzi wa tarafa
wahakikishe askari wa kata wanakuwa katika maeneo yao kila siku hali
ambayo itawasaidia kubaini maeneo tete.
Akiongea katika uzinduzi huo
Diwani wa kata hiyo Rick Moiro alivitaka vikundi hivyo kufuata taratibu
za kazi na kupambana na uhalifu hasa vijana wanaojihusisha na madawa ya
kulevya aina ya bangi huku akiomba Jeshi la Polisi litoe ushirikiano wa
karibu na vikundi hivyo pindi tu wanapoomba msaada.
Naye Afisa Mtendaji wa kata hiyo
Bi. Editha Kisangia alisema kwamba mbali na hali ya uhalifu kuwa ya
kawaida katika eneo hilo lakini hatarajii kutokea kwa changamoto kutoka
kwa baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia vikundi hivyo kwani faida
wataiona baada ya kuanza kufanya kazi.
Wakaguzi wa Polisi wanaoongoza
tarafa tatu za halmashauri ya jiji la Arusha toka mwaka 2013 ni pamoja
na Frimina Massao tarafa ya Suye, Winibrita Moshi tarafa Elerai na
Shabani Shabani tarafa ya Themi.
No comments:
Post a Comment