Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Wednesday, July 27, 2016

ASKARI ALIYEMUUA MWANAHABARI DAUDI MWANGOSI AFUNGWA JELA MIAKA 15


Na MatukiodaimaBlog , Iringa

MAHAKAMA kuu kanda ya Tanzania kanda ya Iringa imemhukumu kwenda jela miaka 15 askari Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia ( FFU )Iringa namba G 58 Pacificius Cleophace Simon (27) kwa kosa la kumuua bila kukusudia mwaahabari Daudi Mwangosi mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi. wakati akiwa katika majukumu yake ya kuchukua habari huku mke wa marehemu Mwangosi Itika Mwangosi akipongeza vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano mkubwa katika kufuatilia kesi hiyo. 


"Mahakama inatambua uchungu wa familia iliyoupata kwa kifo cha marehemu Daudi Mwangosi ambaye aliuwawa pia marehemu aliuwawa kikatili ....siku zote adhabu inapaswa kulingana na kosa husika mahakama haiafiki maombi ya wakili wa upande wa utetezi kuomba mshtakiwa apewe adhabu ya kuachiwa huru kwa kuwa ni yatima ....mgongano wa hisia umeonekana katika kesi hii ila mahakama inampa adhabu ya kwenda jela miaka 15" alisema jaji Dkt Paul Kiwelo.

Akisoma shauri ya kesi hiyo kabla ya kutoa adhabu leo mahakamani hapo jaji Dkt Kiwelo aliwashukuru wazee wa baraza la mahakama kwa michango yao mkubwa mchango ulioisaidia mahakama hadi kufikia siku hiyo ya hukumu pia mawakili wote walioshiriki katika kesi hiyo.

" Suala la aina gani ya adhabu inafaa halikuwa rahisi sana kwani shauri hili upande wa jamhuri uliomba adhabu ya kufungwa maisha jela huku upande wa utetezi ukiomba mshitakiwa aachiwe huru kwa masharti ambayo mahakama ingeona yanafaa kutokana na kuwa na majukumu ya kulea wadogo zake na yeye kuwa yatima .....mahakama imetazama ukubwa wa kosa husika pia jamii ina mtazamo gani katika kesi hiyo lakini mahakama haitoi hukumu kwa mitazamo mbali mbali inatumia vifungu vya sheria suala la kutoa adhabu ni la kisheria si vinginevyo".

Jaji Dkt Kiwelo alisema kuwa adhabu haitolewi kwa ajili ya kulipiza kisasi ila inatolewa kama sehemu ya onyo na kuifanya jamii kutambua kuishi kwa kuheshimu misingi ya sheria kwani kuna mambo manne katika kesi yanatazamwa likiwemo la medhania ya kosa alilotenda na aina ya kosa pia maslahi ya jamii katika kosa husika.

Mjane wa marehemu Daudi Mwangosi akizungumza na wanahabari ikiwa ni pamoja na kuwashukuru kwa umoja wao .


Rais wa umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Bw Deo Nsokolo akizungumza na wanahabari baada ya hukumu ya kesi ya mauwaji ya Mwangosi .

Wanahabari mkoa wa Iringa wakimsikiliza Bw Nsokolo leo





Wanahabari wakiwa nje ya viwanja vya mahakama baada ya kesi kumalizika .


Mjane wa Mwangosi Itika Mwangosi mwenye kilemba akitoka mahakamani hapo huku akiwa na uso wa furaha baada ya hukumu kutolewa kwa muuaji kufungwa miaka 15 jela .

Mjane wa Mwangosi akiwa katika viwanja vya mahakama kuu kanda ya Iringa
Rais wa UTPC Deo Nsokolo akiwa na mtaalam wa IT Lukelo Mwaipopo leo nje ya mahakama kuu kanda ya Iringa
"Naomba kusema mgongano wa hisia umeonekana katika kesi hii pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo bado mahakama haijayumbishwa na migogano hiyo .....mahakama haiitoi hukumu kwa kutazama ni kosa la kwanza wala mhusika hana rekodi mbaya ya makosa mahakama inaendeshwa kwa sheria ndugu wangefurahi kuona mtuhumiwa anafungwa hivyo siafiki maombi ya upande wa utetezi juu ya mkosaji naamini kabisa kwa kosa hili kumwachia kwa Masharti haki haitakuwa imetendeka"




Ndugu wa Marehemu Daudi Mwangosi mama Mfugale kushoto akitoka mahakama kuu kanda ya Iringa akiwa na furaha baada ya hukumu ya kesi hiyo kutolewa leo kwa askari aliyeuwa kufungwa jela miaka 15 Picha zote na MatukiodaimaBlog .

Mjane wa marehemu Daudi Mwangosi Itika Mwangosi mwenye kilemba cheusi akiwa katika foleni ya ukaguzi wa polisi ili kuingia mahakama kuu kanda ya Iringa leo .
Mjane wa marehemu Daudi Mwangosi Itika Mwangosi mwenye kilemba cheusi akiwa katika foleni ya ukaguzi wa polisi .

Mjane wa marehemu Daudi Mwangosi Itika Mwangosi mwenye kilemba cheusi akifurahi jambo na ndugu yake mzee Marko Mfugale mahakamani hapo leo .
Mdogo na marehemu Mwangosi Bw Mecky Mwangosi kulia akisalimiana na Rais wa UTPC Deo Nsokolo kabla ya mahakama kuanza leo

Kwa mujibu wa sheria kuua bila kukusudia ni kosa kubwa sana ambapo adhabu yake huwa ni kufungwa jela maisha japo kila kosa huamuliwa kutokana na mazingira yake hivyo lazima upewe adhabu ambayo itakuwa funzo kwa wengine." Kuua si jambo dogo na mahakama hii kwa kuzingata vifungu vya sheria na pia mtuhumiwa umekaa mahabusu miaka minne inakuhukumu kwenda jela miaka 15 rufaa ipo wazi kwa asiyeridhika".

Akizungumza na wanahabari mara baada ya hukumu hiyo aliyekuwa wakili wa utetezi Lwezaula Kaijage alisema kuwa alisema kuwa yeye alikuwa ni wakili wake na kuwa kwa sasa hawezi kusema ni uamuzi gani ambao mteja wake anaweza kuchukua hadi hapo atakapowasiliana nae .


" Nafikiri wote mlikuwepo mahakamani mmesikia kuwa amefungwa miaka 15 itabidi sasa mimi niende magereza kuzungumza nae ili nichukue sheria nione zinasemaje pia kuomba mwenendo mzima wa sheria kuona jinsi ulivyokwenda ili nione ni kitu gani ambacho labda mahakama ilielekezwa vibaya kabla ya kutoa hukumu hiyo kama nitaona kuna jipya basi tutakwenda kwenye rufaa".

Wakili wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu ((THRDC)Benedict Ishabakaki alisema kuwa katika hukumu hiyo mahakama kuu kanda ya Tanzania kanda ya Iringa imetenda haki pasipo kuegemea upande wowote na kuwa pamoja na nguvu kubwa ya polisi na jinsi ambavyo ushahidi uliokuwa umepelekwa kulenga kumnasua mwenzao ila mahakama hiyo imetumia ushahidi wa ungamo la mlinzi wa amani kutoa hukumu ambayo kimsingi haijaacha maswali kwa wananchi .

Wakili Shabakaki alisema kuwa kesi hiyo polisi waliifanya kama kesi ya nyani kumhukumu ngedele kwa kula mahindi kwani alisema aliyetenda kosa alikuwa ni askari ,mchunguzaji wa kesi hiyo ni askari hivyo katika mazingira hayo haikuwa rahisi kesi hiyo kufikia hukumu hiyo ila mahakama imetenda haki na kuwa wao kama watetezi wa haki za binadamu wataona ni hatua zipi za kuchukua baada ya mahakama kutenda haki .


Alisema pamoja na jukumu la polisi la ulinzi wa jamii ila polisi baadhi yao wameendelea kukiuka wajibu wao na kuogopwa zaidi na raia jambo ambalo si jema na kuwa nguvu kubwa iliyotumika siku zote wakati wa kesi hiyo ni kielelezo tosha kuwa polisi walikuwa wakitegemea mwisho wa siku mwenzao huyo kuachiwa huru . 


Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema kuwa wao kama UTPC wanapongeza mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa kwa kutenda haki katika kesi hiyo kwani alisema kuwa jeshi la polisi walipanda kuharibu kesi hiyo ila jaji kwa umakini wake ametoa adhabu .


" Sisi kama wanahabari tunajipongeza pia kwa hukumu hii kwanza kutiwa hatiani kwa mtuhumiwa na pili kufungwa jela miaka 15....... na ifahamike kuwa kesi hiyo ilikuwa ikiihusu serikali hivyo hukumu ya kesi hiyo imeingia katika rekodi ya dunia kuwa mwandishi aliuwawa na muuaji amefungwa miaka 15 jeshi la polisi Iringa kwa muda wote limekuwa likiwanyanyasa waandishi hivyo sisi kama viongozi wa wanahabari tutakwenda kuonana na viongozi wao wa juu".

Alisema kuwa yapo mambo ya msingi ambayo jeshi la polisi linapaswa kufanya ila si kwa kutumia nguvu kubwa kunyima uhuru wa vyombo vya habari hasa katika kesi hiyo ya Mwangosi .

" Polisi katika kesi nyingine wamekuwa wakiwasaidia wanahabari kupata picha kirahisi kwa watuhumiwa pindi wanapofikishwa mahakamani ila katika kesi hiyo wamekuwa wakimfunika mwenzao na kuzuia waandishi kupiga picha ila pamoja na yote hayo adhabu imetolewa pale pale"

Makamu Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile alisema kuwa polisi Iringa walitamani kuona kesi hiyo inaharibika na kama lisingelikuwa ungamo la mlinzi wa amani mtuhumiwa huyo alikuwa anaachiwa huru na ungamo chini ya mlinzi wa amani ni mahakama yenyewe hivyo ni wazi mahakama imeweza kutenda haki zaidi .


" Adhabu ni kumfanya mtu ajirekebisha na wapo waliotegemea kuwa muuaji wa Mwangosi nae ana hukumiwa kufa ila si haki binadamu ....lakini mtuhumiwa huyo wakati wote wa kesi hiyo hakupaswa kufikishwa mahakamani na polisi wenzake badala ya askari wa magareza ambao ndio wanawajibu wa kumpeleka mahakamani na mahabusu ila .....hata leo baada ya hukumu hatujui amepelekwa wapi maana wameondoka nae wao wenyewe ambao walitaka kesi ivurugike sasa sijui wanampeleka rumande ama gerezani au wamempeleka nyumbani kwanza kula chakula lakini naomba hili kuliacha hapo"

Bw Balile alisema kuwa kwa sasa wanaanzisha mchakato wa kufungua kesi ya madai kwa ajili ya familia ya Mwangosi na kuwa kujua ni mahakama ya ndani ama ya Afrika ambayo kesi hiyo itafunguliwa itajulikana baada ya kwenda kukaa na viongozi wenzake japo alisema haki yote itafikishwa kwa familia ya Mwangosi .

Juzi Julai 25 mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa ilimkuta na hatia askari Simon katika kesi hiyo namba 45 ya mwaka 2013 ya mauaji ya bila kukusudia ya mwahabari Mwangosi aliyeuwawa kinyama Septemba 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi wakati chama cha Demokrasia na maendeleo (chadema) wakifanya uzinduzi wa matawi huku kukiwa na katazo la matukio ya mikutano ama mikusanyiko ya kisiasa kutokana na serikali kuongeza muda wa kuendelea na zoezi la senza ya watu na makazi.

Mjane wa marehemu Mwangosi Bi Itika Daudi Mwangosi alitoa pongezi nyingi kwa wanahabari kwa ushirikiano wao wakati wote wa kesi hiyo hadi ilipofikia mwisho .

" Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutufikisha salama siku hii ya leo .....na niishukuru mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa kwa kuweza kutenda haki pili ninawashukuru sana ninyi waandishi wa habari kwa umoja wenu ...nawashukuru sana tena sana zaidi ya sana hata kama mtu amekutendea wema gani Mungu alitupa neno moja tu la ahsante pia napenda kuwatia moyo msiogope songeni mbele Mungu yu paoja nanyi kama alivyowapigania hadi kufika leo atazidi kuwapigania zaidi teteeni kazi zenu elimisheni jamii vile mnavyoendelea kusaidia jamii ndivyo Mungu anavyowabariki daima sina neno la zaidi zaidi ya ahsante ".


Marehemu Daudi Mwangosi aliuwawa kinyama Septemba 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wakati wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) kilipokuwa kikifanya mikutano ya ufunguzi wa matawi wakati kukiwa na zuio la mikutano hiyo kutokana na kuongezwa kwa muda wa senza ya watu na makazi .

No comments:

Post a Comment