Picha zote na Raymond Mushumbusi MAELEZO
……………………………………………………………………………………………
Na Jacquiline Mrisho Maelezo
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais,TAMISEMI, Mhe.George Simbachawene amewataka Wakuu wa Mikoa
walioapishwa kufanya kazi kwa bidii na kutumia muda mwingi kutatua kero
zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Mhe.Simbachawene ameyasema hayo
leo Jijini Dar es salaam alipokutana na Wakuu hao wa Mikoa ambapo
amewasisitiza kwenda na kasi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili
kutimiza malengo yaliyopangwa katika uongozi wa Serikali ya awamu ya
tano.
“Mfumo wa sasa wa uongozi ni
tofauti na mfumo wa zamani, namna Mhe. Rais anavyotaka tufanye kazi ni
tofauti na zama zingine zilizopita,Wakuu wa Mikoa mnapaswa kujua kila
kinachoendelea kila siku katika Mikoa yenu na mnapaswa muwajibike kwa
wananchi wenu”alisema Simbachawene.
Mhe.Simbachawene ameongeza
kuwa,Wakuu wa Mikoa wamepewa madaraka ya kusimamia mfumo wa ufanyaji
kazi kwa kuhakikisha watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo kwakua nchi
haiwezi kubadilika kama hakutakua na utendaji mzuri.
Aidha,Mhe.Simbachawene
amewakumbusha Wakuu wa Mikoa wazingatie na kusimamia haki za wananchi
kwakua kuna baadhi ya mamlaka za Serikali za Mitaa zinaripotiwa kuwaonea
sana wananchi hasa wanawake katika kupata haki zao maana ndio
wanaongoza kwa kunyanyaswa.
Pia amewataka Wakuu wa Mikoa
kutumia mamlaka waliyopewa kuvunja mabaraza yote ya usuluhishi
yasiyozingatia sheria katika kutoa maamuzi na kuunda mabaraza mapya
yenye sifa za kutatua kesi za wananchi.
Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais,TAMISEMI, Mhe. Selemani Jaffo ameahidi kuwapa Wakuu wa Mikoa
ushirikiano wa kutosha kutoka Ofisi ya TAMISEMI ili kuhakikisha kazi zao
zinafanyika kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment