Moja ya gari lililopata ajali katika msafara wa Waziri Suleiman Jafo.
……………………………………………………………………………………………………
Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) leo imepokea majeruhi watano wa ajali ambayo imetokea katika eneo
la Kerege wilayani Bagamoyo mkoani Pwani iliyohusisha wafanyakazi wa
Halmshauri ya Bagamoyo wakiwa na baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Bunge,
Utawala na Tamisemi kama ilivyoripotiwa na mitandao mbalimbali ya
kijamii.
Pia, Hospitali imepokea mwili wa
mtu mmoja ambaye amefariki dunia wakati akiletwa hospitali hapa
aliyefahamika kuwa ni Juliana Masaga ambaye alikuwa mhandisi wa maji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
Majeruhi waliopokelewa ni pamoja
na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ibrahim Matovu, Julius Mwanganda
ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii, George Mashauri Mweka Hazina, Doroth
Njitile, mratibu wa TASAF na Tanwira Khalid ambaye ni raia.
Kati ya majeruhi hao, Doroth
amefanyiwa upasuaji baada ya kuumia kifua, sehemu za miguu na tumbo.
Majeruhi wengine wanne wameumia sehemu za miguu na kuhamishiwa Taasisi
ya Tiba ya Mifupa (MOI).
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amefika kuwajulia hali majeruhi kwenye hospitali hiyo leo. Hata
hivyo kutokana na maadili ya kutoa huduma kwa wagonjwa walioko eneo la
dharura hatukupiga picha wakati wakihudumiwa.
No comments:
Post a Comment